Baridi inayonikabili ni ja kimiujiza. Mwili wangu umelemwa na kubadilika mithili ya barafu yenyewe. Kisa changu kinaanzia kwenye kituo cha basi kilichoko karibu na nyumba niishiyo. Nilikuwa nimerudi nyumbani baada ya siku ndefu shuleni, isitoshe kijitihani cha hesabu. Ilinibidi kwanza nitume barua pepe kadhaa kwa jamaa na marafiki ambao walikuwa wameniandikia hapo awali lakini nikawa sina fursa ya kuzijibu barua zao. Baadaye nilijitayarishia chakula na kilikuwa si kingine bali 'pasta'.
Nilipokuwa nikila ndipo nilikumbuka kwamba ilinibidi nirudi shuleni kabla ya saa kumi na nusu ili nikalipe ada ya shule ya muhula huu. Nililiva koti langu la buluu na kuyateremka madaraja. Niliufungua mlango mkuu, nikatupa jicho kituoni na nikajikokota huko. Hapakuwa na mtu mwingine ila mimi huko. Theluji iliyokuwa nje na bado iko nje ni nyingi, kiasi kwamba inaweza kufunika kiatu chako na zaidi. Baridi nayo ilikuwa nyingi nikasikia mfano wa jiwe la barafu. Si suruali yangu ndefu si glavu, zote zilikuwa baridi mithili ya barafu. Hapo ndipo nilipokumbuka Mombasa, Kenya. Laiti ningalikuwa Mombasa kwenye ufuko wa bahari Idi, ningalifurahia jua, maji ya chumvi na hata ya mnazi.
Lakini jambo la kuhuzunisha ni kwamba huku nimekwama. Nitakapoondoka sijui na hata unkiniuliza siwezi kukuambia; sifahamu. Hata hivyo najituliza moyoni kwani miezi michache kutoka sasa theluji itakuwa ni jambo la historia na jua itakuwa ndio siasa.
Thursday, February 1, 2007
Subscribe to:
Posts (Atom)